Sudan itaacha mafuta ya Juba kupita

Serikali ya Sudan imesema itaruhusu shehena ya mafuta ya Sudan Kusini kusafirishwa, katika juhudi za kuzimua ugomvi baina ya nchi mbili hizo.

Mkutano wa dharura unaofanywa Addis Ababa, ulishindwa kupata ufumbuzi Ijumaa.

Sudan Kusini inasema inakaribia kumaliza shughuli za kusitisha uchimbaji wa mafuta, ambayo inapitisha Sudan Kaskazini hadi bandarini.

Sudan inasema itaruhusu meli zilizosheheni mafuta ya Sudan Kusini, ilizokuwa imezizuwia katika bandari ya Port Sudan.

Sudan Kusini imeishutumu Sudan Kaskazini kuwa imechukua mafuta yenye thamani ya dola milioni 815.

Afisa mwandamizi wa Sudan Kaskazini aliwaambia waandishi wa habari mjini Addis Ababa, kwamba kuziachia meli hizo kusafiri kutafungua milango ya kupata ufumbuzi na makubaliano baina ya nchi mbili hizo kutiwa saini.

Sayed el Khatib alisema serikali iko tayari kutia saini makubaliano hii leo.

Jana jioni, kiongozi wa ujumbe wa Sudan Kusini, Pagan Amum, alisema makubaliano hayakupatikana kwa sababu Sudan Kaskazini inaiba mafuta ya Sudan Kusini.

Na alisema uzalishaji mafuta utasimamishwa kabisa.

Ikiwa mafuta hayatachimbwa, nchi zote mbili zitaumia - Sudan Kusini itakosa pato la kuuza mafuta ambayo lazima yapite kaskazini kwa vile nchi hiyo haina bandari.

Na Sudan Kaskazini inahitaji pato kutoka kuruhusu mafuta hayo kupita katika ardhi yake.