Wageni wapunguza msaada kwa jamaa

Wakati viongozi wa Afrika wanakutana kujadili namna ya kuzidisha biashara, baadhi ya mabenki makuu ya Afrika yameonya kuwa kuzorota kwa uchumi katika bara la Ulaya kumepunguza kiwango cha fedha ambazo wafanyakazi wa kigeni wanaweza kuwatumia jamaa zao nyumbani.

Haki miliki ya picha Reuters

Mwezi uliopita shirika la msaada la Oxfam lilisema pesa ambazo wageni walioko Ulaya wanapeleka kusaidia nyumbani zimepungua, na ndio sababu moja ya shida za chakula katika eneo la Sahel la Afrika.

Huo ni mfano mmoja unaoonesha umuhimu wa mishahara ya wafanyakazi wa kigeni walioko Ulaya, kwa nchi za Afrika.

Umoja wa Mataifa unasema kawaida msaada wa wageni unachangia asili-mia-5 ya pato la mataifa ya Afrika.

Pesa hizo zinasaidia sana familia, hasa zile zilioko mashambani, kwa kulipia siyo tu chakula lakini piya matibabu na elimu.

Msaada wa kimataifa na uwekezaji unaweza kuzidi au kupungua, lakini msaada wa wageni kwa jamaa zao umekuwa ukizidi taratibu kwa miaka 10 iliyopita.

Sasa wakuu wa benki kuu za Burundi na Uganda wameonya kuwa msaada huo unapungua.

Gavana wa benki kuu ya Burundi, Gaspard Sindayigaya, anasema anaendelea kuchunguza hali hiyo.