Senegal: Maandamano kufanyika leo

Rais wa Senegal Abdoulaye Wade Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Rais wa Senegal Abdoulaye Wade

Nchini Senegal, kikundi kinachojiita M23 kimeitisha mkutano hii leo jijini Dakar wakitaka Rais Abdoulaye Wade kutowania urais katika uchaguzi utakaofanyika Februari tarehe 26.

Jina lake liliidhinishwa na baraza la katiba. Wanachama wa baraza hilo walichaguliwa na Rais Wade mwenyewe. Maandamano haya yatafanyika wakati ambapo kuna wasiwasi nchini humo.

Serikali nchini Senegal imeonekana kutotaka machafuko yoyote kutokea. Usalama tayari umeimarishwa karibu na makao ya Rais Abdoulaye Wade, bunge la nchi hiyo na majengo muhimu jijini Dakar. Hapo jana, polisi wa kupambana na ghasia walishika doria wakiwa kwenye magari na wakiwa wamebeba vitoa machozi.

Wasiwasi unasemakana kutanda jijini Dakar na maeneo mengine nchini Senegal. Siku ya Jumatatu, watu wawili waliuawa eneo la Podor, kaskazini mwa Senegal, wakati wa maandamano ya kupinga uamuzi wa kumruhusu Rais Abdoulaye Wade kugombea urais kwa kipindi cha tatu . Waandamanaji kadhaa waliojeruhiwa wamepata matibabu katika hospitali.

Mtu mmoja aliyeshuhudia maandamano hayo aliimbia BBC kwamba watu wameghadhabishwa na maafisa wa usalama na kwamba vikundi vya vijana vimeamua kupambana nao leo. Ijumaa iliyopita, afisa mmoja wa polisi aliuawa na waandamanaji jijini Dakar .

Wanaompinga Rais Wade wanasema katiba inaeleza wazi kwamba kiongozi hafai kuwania urais kwa zaidi ya mihula miwili. Lakini Bwana Wade na wanaomuunga mkono wanasema katiba ilibadilishwa baada ya uchaguzi wa urais na hivyo sheria ya kuwania urais mara mbili tu haimfungi kwa njia yote ile. Anasema sheria hii itatekelezwa kwa marais watakaofuatia. Rais Wade ameitawala Senegal kwa muda wa miaka kumi na miwili.

Ufaransa, Marekani na jumuiya ya ulaya zimeeleza wasiwasi wao kwamba nchi hiyo inaweza kukumbwa na ghasia. Serikali za ulaya zimewaonya raia wao walioko Senegal kuwa waangalifu.