Mabomu ya machozi yavurumishwa Misri

Ghasia Haki miliki ya picha Getty
Image caption Ghasia baada ya mechi

Waandamanaji waliokasirishwa na vifo vya watu 74 baada ya mchezo wa kandanda katika mji wa Port Said nchini Misri siku ya Jumatano wamepambana na polisi nje ya wizara ya mambo ya ndani mjini Cairo.

Kituo cha TV cha serikali kimesema mamia ya watu wamejeruhiwa katika tukio hilo.

Mapema, waziri mkuu wa Misri alitangaza kuwafukuza kazi maafisa wa ngazi za juu mjini Port Said na pia katika chama cha soka cha Misri.

Mazishi ya baadhi ya waliokufa yamefanyika katika mji wa Port Said.

Vizuizi

Ghasia za siku ya Jumatano, zilianza baada ya mashabiki kuvamia uwanja kufuatia kumalizika kwa mechi ya soka kati ya klabu ya Cairo, al-Ahly na klabu ya Port Said, al-Masry.

Mjini Cairo, watu walikusanyika katika mitaa kuzunguka eneo la wazi la Tahrir, aneo ambalo lilikuwa kitovu cha maandamano yaliyosababisha kuondoka madarakani kwa Rais Hosni Mubarak mwaka jana.

Waandamanaji hao, wengi wao wakiwa mashabiki wa al-Ahly maarufu kwa jina la Ultras, walitumia vyuma na magari kuweka vizuizi karibu na eneo hilo la wazi.

Maelfu ya waandamanaji hao walikwenda katika wizara ya mambo ya ndani iliyopo umbali wa mita 500. Baadhi yao waliimba nyimbo kushutumu watawala wa kijeshi wa Misri, huku wengine wakirusha mawe.

Polisi walijibu mashambulizi kwa kurusha mabomu ya kutoa machozi na kusababisha mamia kukimbia.

Kimya

Pikipiki zilisafirisha majeruhi kutoka eneo la tukio kwa kuwa magari ya kubebea wagonjwa hayakuweza kupita.

Kituo cha TV cha taifa kimesema watu 382 walijeruhiwa, kati yao 266 wakipelekwa hospitali, huku wengine wakitibiwa katika eneo la vurugu.

Picha za televisheni kutoka Cairo zimeonesha umati wa watu nje ya vizuizi vinavyozunguka wizara ya mambo ya ndani.

Mapema siku ya Alhamis, bunge lilikutana katika kikao cha dharura, na kuanza kwa kukaa kimya kwa dakika moja.

Waziri Mkuu Kamal al-Ganzouri aliwaambia wabunge kuwa mkuu wa chama cha soka cha Misri amefukuzwa kazi na bodi ya chama hicho kufutwa, na wajumbe wake wote kufikishwa kwa waendesha mashtaka kwa ajili ya kuhojiwa.

Mkurugenzi wa usalama wa Port Said na mkuu wa uchunguzi walisimamishwa kazi na wanashikiliwa na polisi, amesema Bw Ganzouri.

Mwandishi wa BBC Jon Leyne aliyepo mjini Cairo amesema kuna hali ya hasira kali. Mashabiki wengi wanaamini polisi hawakuwajibika vilivyo, au walichochea ghasia hizo.

Polisi nchini Misri wamekuwa 'wapole' tangu kutokea kwa maandamano ya mwaka jana.

Wakati huohuo, kundi la Muslim Brotherhood ambalo limeibuka na ushindi katika uchaguzi wa hivi karibuni limetupia lawama wafuasi wa rais wa zamani Hosni Mubarak kwa ghasia hizo.