Msemaji wa Boko Haram akamatwa

Mkubwa wa Boko Haram aliyeuawa, Mohammed Yusuf
Image caption Mkubwa wa Boko Haram aliyeuawa, Mohammed Yusuf

Polisi nchini Nigeria wamemkamata msemaji wa kundi lenye itikadi kali la Boko Haram ambalo limetekeleza mashambulio kadhaa hivi karibuni.

Afisa wa polisi alisema jamaa huyo , anayejulikana kwa jina la bandia kama Abul Qaqa, alikamatwa katika mji wa Maiduguri katika jimbo la Borno.

Afisa huyo aliliambia shirika la habari la Associated Press kwamba msemaji huyo alikamatwa baada ya polisi kumfuatilia wakitumia simu yake.

Zaidi ya watu 150 waliuawa na kundi la Boko Haram mwezi uliopita; milipuko kadhaa iliporomosha majengo ya polisi na ofisi za uhamiaji katika mji wa Kano.

Lilikuwa shambulio baya zaidi kuwahi kutekelezwa na kundi hilo.

Kundi hilo limesema linataka kupindua serikali ya Nigeria na badala yake kuhakikisha nchi hiyo inatawaliwa kwa mujibu wa sheria za kiislamu.

Wanachama wa kundi hilo wameshambulia vituo vya polisi na majengo mengine ya serikali na pia kulipua makanisa na kuwaua mamia ya watu wakiwemo Wakristo na Waislamu.