Jeshi la Kenya lateka mji wa Badhadhe

Jeshi la Kenya limesema limefanikiwa kuuteka mji mmoja muhimu kusini mwa somalia kutoka kwa wapiganaji wa kiislamu wa al-shabaab.

Haki miliki ya picha internet
Image caption Wanajeshi wa Kenya

Msemaji wa jeshi la Kenya Major Emmanuel Chirchir ameiambia bbc kuwa majeshi yake yameuteka mji wa Badhadhe, hatua ambayo ameitaja kama pigo kubwa kwa wapiganaji hao wa Kiislamu.

Duru kutoka mji huo zinasema kuwa wanajeshi wa Kenya wakisaidiana na wapiganaji wa kundi la wanamgambo wanaoiunga mkono serikali ya mpito nchini Somalia, waliuteka baada ya mapigano makali.

Msemaji wa jeshi la Kenya, meja Emmanuel Chirchir, amesema kuwa kutekwa kwa mji huo ni pigo kubwa kwa kundi la wanamgambo la al-shabaab.

Hatua hiyo ina maana kuwa njia waliokuwa wakitumia kutoka baharini kuingia nchi kavu sasa imezibwa.

Major Chirchir kadhalika amesema kuwa mji huo wa Badhadhe ulikuwa muhimu sana kwa wanamgambo hao kwa kuwa ulitumiwa kutoa mafunzo ya kivita.

Mara kadhaa serikali ya Kenya imezungumzia ushindi wake wa kuteka miji kadhaa. Mafanikio yao mengi hata hivyo yamekuwa ni kuteka miji midogo tu.

Hata hivyo utekaji wa mji wa Badhadhe ni hatua kubwa kwa sababu ni makao makuu ya wilaya katika eneo la Juba ya chini.

Majeshi ya Kenya yaliingia Somalia Octoba mwaka uliopta na serikali ilisema kuwa lengo lilikuwa ni kupambana na kundi la Al- shabaab ambalo lilidaiwa kutekeleza utekajinyara wa wageni wa kigeni ndani ya Kenya.

Inaaminika lengo kuu la majeshi ya Kenya ni kuuteka mji wa Kismayu ulioko pwani ya Somalia.