Malaria inasababisha vifo vingi zaidi

Mbu Haki miliki ya picha Sam CottonUCL
Image caption Mbu

Matokeo ya utafiti mpya yaliyochapishwa katika jarida la matibabu la Lancet, yamebainisha kuwa ugonjwa wa Malaria husababisha vifo vya watu wengi duniani kuliko ilivyokisiwa.

Wanasayansi nchini Marekani na Australia wanasema watu milioni 1.2 waliaga dunia mwaka wa 2010 kutokana na kuugua ugonjwa wa Malaria; idadi ambayo ni asilimia 100 zaidi kuliko ilivyokadiriwa na shirika la umoja wa mataifa la afya duniani WHO.

Wanasayansi hao wanasema zaidi ya asilimia 40 ya waliokufa ni watoto walio na umri zaidi ya miaka mitano na watu wazima na hivyo kuhoji imani kuwa idadi kubwa ya vifo vinavyosababishwa na ugonjwa huo huathiri watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano.

Watafiti hao wanasema takwimu hizo zimetokana na takwimu mpya na mbinu mpya ya kuorodhesha vifo ambavyo hapo awali vilikisiwa kusababishwa na magonjwa mengine.

Mhariri wa jarida hilo la Lancet, Richard Horton, aliiambia BBC kwamba katika muongo mmoja uliopita, ni watu milioni 230 wametibiwa kutokana na ugonjwa wa Malaria na idadi sawa ya vyandarua vilivyosambazwa kwa watu walio katika hatari ya kuambukizwa ugonjwa huo.