Zambia yaibandua Ghana Kombe la Afrika

Zambia imeifunga Ghana 1-0 Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Zambia imeifunga Ghana 1-0 na kufuzu fainali ya Kombe La Mataifa ya Afrika.

Zambia imeifunga Ghana 1-0 na kufuzu fainali ya Kombe la mataifa ya Afrika kwenye mechi ya nusu fainali mjini Bata, Equatorial Guinea.

Mshambuliaji Emmanuel Mayuka ambaye aliingia kipindi cha pili ndiye aliyeifungia Zambia bao la ushindi katika dakika ya 78.

Mshambuliaji wa Ghana Asamoah Gyan alikosa penalti katika dakika ya 8 kipindi cha kwanza.

Ghana walimaliza wachezaji 10 baada ya Derek Boateng kupewa kadi nyekundu kuelekea mwisho wa mechi.

Mayuka ni mchezaji pekee katika timu ya Zambia anayecheza soka ya kulipwa ulaya.

Zambia haijapata kushinda Kombe la mataifa ya Afrika, lakini mara mbili wamefika fainali, na sasa wamefuzu fainali mara ya kwanza tangu mwaka 1994.