Nigeria: Nuhu Ribadu apata cheo kipya

Nuhu Ribadu mwenyekiti wa tume ya sekta ya mafuta
Image caption Nuhu Ribadu mwenyekiti wa tume ya sekta ya mafuta

Aliyekuwa mkuu wa tume ya kupambana na ufisadi nchini Nigeria Nuhu Ribadu amesema anakiona cheo chake kipya cha mwenyekiti wa tume ya kufuatilia na kuchunguza shughuli za sekta ya mafuta nchini humo kama huduma kwa taifa.

Timu yake ya watu 21 itafuatilia fedha zinazolipwa kwa serikali na kuchunguza na kufuatilia uzalishaji na mauzo ya mafuta yasiyosafishwa.

Mwaka jana Bwana Ribadu aliwania urais lakini akashindwa na Goodluck Jonathan, ambaye amemteua kushika cheo hicho kipya.

Bwana Ribadu amesema kwamba licha ya tofauti za kisiasa, watu wote nchini Nigeria wanakubaliana kwamba ufisadi unaathiri vibaya nchi hiyo.

Nigeria ndiyo nchi ambayo inaongoza katika uzalishaji wa mafuta barani Afrika lakini sekta ya mafuta imekumbwa na madai ya ufisadi ; jambo ambalo wengi wanasema linasababisha raia wengi wa nchi hiyo kubaki maskini.

Mwandishi wa BBC Chris Ewokor, ambaye yuko Abuja, anasema hii ni mara ya kwanza kwa tume kuteuliwa kufuatilia shughuli za sekta ya mafuta.