Sudan na Sudan Kusini zakutana Addis

Mafuta Sudan Kusini Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mafuta Sudan Kusini

Sudan na Sudan Kusini zitarejea katika mazungumzo mjini Addis Ababa, Ethiopia, leo.

Nchi hizo mbili zimekuwa katika mzozo uliosababishwa na mapato ya mafuta na kwa sehemu ya uamuzi wa Sudan Kusini kusitisha uzalishaji wa mafuta yake.

Sudan Kusini ilipata uhuru wake kutoka Sudan, Khartoum mwezi Julai mwaka jana, huku masuala mengi yanayozihusu nchi mbili hizo jirani yakiwa hayajapatiwa ufumbuzi.

Mwezi uliopita, Sudan Kusini ilifunga uzalishaji wa mafuta yake, baada ya kuishtumu Sudan kaskazini kuiba mafuta hayo.

Sudan kusini ilikuwa ikisafirisha nje mafuta yake hayo kupitia bomba la jirani yake Sudan kaskazini, lakini hapakuwa na makubaliano yoyote kuhusu ushuru wa kupitishia mafuta hayo.

Wanaharakati wa shirika la Global Witness wametaka Muungano wa Afrika, China na serikali za magharibi kuzishinikiza Sudan na Sudan kusini kumaliza tofauti zao.