Iran yaacha kuuza mafuta Ulaya

Wizara ya mafuta ya Iran inasema kuwa imeacha kuziuzia mafuta Ufaransa na Uingereza, kulipiza vikwazo vilivowekwa na Umoja wa Ulaya dhidi ya mafuta ya Iran kuanzia mwezi wa Julai.

Msemaji wa wizara hiyo, alisema Iran badala yake itauza mafuta yake kwa wateja wepya.

Mapema mwezi huu, Waziri wa Mafuta wa Iran, alisema mafuta yataacha kupelekwa nchi za Ulaya, kabla ya vikwazo kuanza, lakini hakuzitaja nchi gani zitalengwa.

Umoja wa Ulaya na Marekani hivi karibuni ziliweka vikwazo vikali vipya dhidi ya Iran, na kuishutumu kuwa inatengeneza silaha za nuklia, kisirisiri.

Iran inasema kuwa mradi wake wa nuklia ni wa amani.