Misri yavunja uhusiano na Syria

Misri imetangaza kuwa inamuondoa balozi wake mjini Damascus, huku malalamiko yakizidi kuhusu utumiaji nguvu nchini Syria.

Haki miliki ya picha Reuters

Hii ni hatua ya karibuni kabisa, katika kuitenga Syria kimataifa, lakini piya inaonesha maoni ya wengi nchini Misri.

Misri ndio nchi ya Kiarabu ya karibuni kabisa kumuondoa balozi wake mjini Damascus, kulalamika juu ya hatua za serikali ya Syria dhidi ya waandamanaji.

Hatua hiyo ni sehemu ya uamuzi wa kimataifa za kuitenga serikali ya Rais Assad, na ni ishara muhimu.

Zama za siasa za kizalendo za Warabu, nusu karne iliyopita, nchi mbili hizo ziliungana kwa muda mfupi, chini ya uongozi wa Gamal Abdul Nasser.

Hatua ya serikali ya Misri piya inaitikia chagizo nchini, kwamba ioneshe ukali.

Kumefanywa maandamano kadha mjini Cairo nje ya ubalozi wa Syria.

Wakati mmoja waandamanaji waliukalia ubalozi huo kwa muda.

Waandamanaji na chama cha Muslim Brotherhood, chama kikuu bungeni, wametaka balozi wa Syria nchini Misri afukuzwe, lakini hilo bado halikutokea.