Iran yainyima Uingereza mafuta

Iran imesema imesitisha mauzo ya mafuta yake kwa nchi za Ufaransa na Uingereza katika kulipiza kisasi kutokana na uamuzi wa Umoja wa Ulaya kupiga marufuku ununuzi wa mafuta ya Iran utakakoanza kutekelezwa mwezi Julai mwaka huu.

Haki miliki ya picha bbc
Image caption Rais Ahmedinejad wa Iran

Msemaji wa Iran amesema badala yake mafuta hayo watauziwa wateja wapya.

Vyombo vya habari vimesema huenda uamuzi wa Iran dhidi ya nchi hizo usiwe na madhara makubwa kutokana na ukweli kwamba mwaka jana Ufaransa iliagiza kutoka Iran asilimia tatu tu ya mafuta iliyohitaji, huku Uingereza ikiagiza chini ya hapo.

Umoja wa Ulaya unaimarisha vikwazo dhidi ya Iran kwa sababu ya wasiwasi kwamba nchi hiyo inatengeneza silaha za nyuklia, madai ambayo imekanusha.

Hii ni hatua nyengine ya kulipiza kisasi katika vita baridi vinavyoendelea kati ya Iran na mataifa ya Ulaya.

Viongozi wa Iran wanasema uuzaji wa mafuta yao kwa makampuni ya Uingereza na Ufaransa umesitishwa na mafuta hayo yatapata soko kwingineko duniani.

Ugiriki , Uhispania , na Italia ni miongoni mwa mataifa yanayotegemea sana mafuta ya Iran.

Hatua hii ya Iran inaelekea kuupiku Umoja wa Ulaya na Marekani ambao walikuwa wameshatangaza kwamba watasitisha ununuzi wa mafuta ya Iran kuanzia mwezi Julai mwaka huu kama njia mojawapo ya kuishinikiza Iran kuachana na harakati zake za kujenga mitambo ya nguvu za nuklia.

Madai ambayo yamekanushwa na Iran.