Jeshi A Kusini kudhibiti ujangili wa faru

Image caption Faru ujangili waongezeka Afrika Kusini

Afrika Kusini itasambaza mamia ya askari wa ziada katika mipaka yake kusaidia kupambana na makundi ya ujangili wa pembe za faru, serikali imetangaza.

Waziri wa sheria Jeff Radebe alisema vikosi vinne vya kijeshi vitatumwa katika mipaka ya Zimbabwe, Swaziland na Lesotho.

Kuna mitandao ya usafirishaji wa pembe kutoka Afrika na baadhi ya sehemu za Asia na mashariki ya kati.

Mwaka 2011, Afrika Kusini ilifikia rekodi ya faru 450 waliouawa na majangili, Kitengo cha Masuala ya Mazingira kimesema.

Bw Radebe alisema kiasi cha askari 600 watajiunga na vita dhidi ya ujangili wa faru.

"Kundi hilo la askari litakuwa na wahandisi ambao wanafanya ukarabati na matengenezo wa seng’enge katika mpaka wa Zimbabwe-Msumbiji ambao unakaribia kilometa 140 (mile 85) " alisema Bw Radebe.

Mwaka jana vikosi ilipelekwa katika mpaka wa Msumbiji wengi wao katika hifadhi ya Taifa maarufu ya Kruger ambako faru 200 waliuawa.

"Udhibiti mzuri wa mipaka ni sehemu ya mbinu zinazotumika kuzuia uhalifu, ambayo inasaidia kupambana na makundi ya mitandao na kuzuia ujangili." alisema Radebe.

Idadi ya faru waliouawa Afrika Kusini imeongezeka katika miaka ya karibuni kutokana na mahitaji ya pembe zake katika utamaduni wa dawa za asili za Asia has China na Vietnam, ambako zinadhaniwa kuwa na uwezo wa kuponya.

Lakini wanasayansi wanasema pembe za faru zimetengenezwa kwa chembechembe sawa na za kucha na hakuna uhakiki wa kisayansi wa kuwa na dawa.

Bado mahiyaji yake yameongezeka kila mwaka, bei katika soko lisilo rasmi ya pembe za faru sasa katika ukanda huo ni £35,000 ($55,000) kwa kilo.

Afrika Kusini imekuwa ni kitovu cha biashara ya pembe za faru kwa sababu ina asilimia kati ya 70 na 80 katika idadi ya faru wote duniani kiasi cha faru 20,000.

Serikali ya nchi hiyo imeagiza ufanyike utafiti wa iwapo biashara hiyo ihalalishwe kupunguza ujangili.