Sudani Kusini yakata nusu ya matumizi

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Sudan Kusini yakata matumizi yake kwa nusu kufidia mapato ya mafuta

Sudan Kusini imekata bajeti yake ya matumizi kwa nusu katika kila sekta isipokuwa mishahara ili kufidia pengo la mapato ya mafuta kufuatia kufungwa kwa usafirishaji wa mafuta hayo kutokana na mgogoro na Sudan.

Mafuta yanachangia hadi 98% ya bajeti baada ya kujitenga kutoka Kaskazini mwaka jana.

Hakutakuwa na kupunguzwa kazi na mishahara ya serikali bado italipwa, waziri wa fedha alisisitiza.

Rais Salva Kiir alisema taifa lake ni bora lipate shida kwa muda kuliko kuendelea kutoa mapatao yake ya mafuta kwa adui yake mjini Khartoum.

Mabomba ya mafuta yanatokea Sudan Kusini kuelekea kwa jirani yake Kaskazini ambaye walipigana naye vita vikali kwa miongo mingi na kusababisha vifo vya watu wapatao 1.5 millioni.

Lakini nchi hizo mbili hazijafikia muafaka juu ya namna Kusini itakavyolipa.

Mwezi Januari Sudan Kusini ilifunga uzalishaji wote wa mafuta wa mapipa 350,000 kwa siku baada ya Sudan kuanza kuchukua mafuta hayo kufidia kile ilichokiita gharama za usafirishaji ambazo hazijalipwa.

Baada ya Taifa hilo jipya kufunga uzalishaji wa mafuta, Rais wa Sudan Omar al-Bashir alijibu kwa kusema vita ilikuwa karibu zaidi kuliko amani.

Kila upande unautuhumu mwingine kwa kuunga mkono waasi na kumekuwa na mapigano karika mipaka mipya.

'Haraka na ya Kina'

Hatua hizi za kubana matumizi ni za mara moja.

"Huu ni ukataji wa matumizi wa haraka na mkali lakini hatutagusa watumishi wa serikali, au jeshi [wapiganaji wa SPLA," Waziri wa Fedha Kosti Manibe alisema katika taarifa yake Jumapili.

"Mishahara ya kila mmoja iko palepale" alisema.

Mwandishi wa BBC James Copnall mjini Khartoum sanasema hizi ni habari njema kwa mamia ya maelfu ya wafanyakazi na wanaume na wanawake wenye sare.

Bajeti ya kwanza ya Sudan Kusini imetenga zaidi ya 40% ya $2bilioni (£1.2bn) kwa mishahara, shirika la habari la AFP limeripoti.

Mwandishi wetu anasema kuyaacha mafuta ardhini imekuwa ni mbinu maarufu ya Sudan Kusini watu wengi wanaona ni wakati huu sasa nchi inakuwa huru kwelikweli.