Kenny Dalglish aipatia Liverpool kombe

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Kenny Daglish aipatia Liverpool kombe la Carling akiwa kocha

Kenny Dalglish amepata kombe la kwanza tangu arejee kwa awamu ya pili kama kocha wa Liverpool baada ya ushindi wa mikwaju ya penalti dhidi ya Cardiff City katika fainali ya kombe la Carling.

Anthony Gerrard alikosa mkwaju wa mwisho na kuikabidhi Liverpool kombe lake la kwanza tangu washinde kombe la FA mnamo mwaka 2006 - kipigo kilikokua na machungu mengi kwa Cardiff.

Cardiff walifungua mlango kupitia Joe Mason na kulinda lango lao vyema hata baada ya Martin Skrtel kusawazisha.

Dirk Kuyt alidhani ameipatia ushindi Liverpool katika kipindi cha ziada lakini Ben Turner alisawazisha katika dakika ya mwisho ya kipindi cha ziada.

Hata hivyo hatimae haikua ushindi rahisi kwa Liverpool baada ya nahodha Steven Gerrard ambae ni binamu wa Anthony kukosa penalti pamoja na Charlie Adam. Lakini wakafunga mikwaju mitatu kupitia Kuyt,Glen Johnson na Downing. Cardiff walifunga mikwaju miwili tu kati ya mitano.

Dalglish anasema ushindi wa Liverpool ni hatua ya mwanzo tu katika safari ndefu ya kuirejeshea klabu hiyo hadhi yake ya jadi ya kutawala kandanda Uingereza.