Senegal yaelekea duru ya pili ya Uchaguzi

Haki miliki ya picha
Image caption Bw Macky Sall analeta upinzani mkali kwa Rais Wade

Mchuano mkali unaendelea katika uchaguzi wa Urais wenye utata nchini Snegal kati ya Rais wa sasa Abdoulaye Wade na waziri mkuu wa zamani Macky Sall.

Taarifa za awali kutoka Senegal ambazo hazijathibitishwa zinaonyesha kuwa kuna mchuano mkali kati ya Rais wa sasa Abdoulaye Wade na waziri mkuu wa zamani Macky Sall na vyombo vya habari vya ndani na Bw Sall vinasema hakuna mgombea aliyefikia 50% inayotakiwa kuepuka duru ya pili.

Rais Wade, 85, anawania kwa awamu ya tatu nafasi hiyo licha ya kutumikia vipindi viwili vinavyoruhusiwa na katiba.

Bw Wade alizomewa wakati alipokwenda kupiga kura Jumapili katika mji mkuu,Dakar.

Walisikika wakipiga kelele: "toka huko, mzee wewe!"

Uamuzi wa Bw Wade wa kusimama tena umesababisha wiki kadhaa za ghasia na vifo vya watu sita ingawa siku yenyewe ya kupiga kura ilikuwa nay a amani kwa sehemu kubwa.

Taarifa za awasli zinaonyesha kuwa Bw Wade na Bw Sall wote wamepata ushindi kati ya kura 20-35%.

Tume ya uchaguzi haijathibitisha bado matokeo hayo ya awali ambayo yametangazwa na vyombo vya ndanikamayanavyoletwa kwenye vituo vya kupigia kura.

Bw Wade alipoteza kura kwenye jimbolakemwenyewekatika eneo la watu wa kati mjiniDakarjirani na Kituo E, Shirika la Habari la Senegal APS limeripoti.

Mchuano kati ya Abdoulaye Wade na Macky Sall

Abdoulaye Wade

  • Umri: 85
  • Mgombea mkongwe wa upinzani
  • Alichaguliwa mara ya mwisho mwaka 2000,kwa ahadi za mabadiliko
  • Ana mipango mikubwa ya miradi ya kuindeleza Senegal
  • Anatuhumiwa kumuandaa mwanawe, Karim, kuchukua nafasi yake

Macky Sall

  • Umri: 50
  • Meya wa mji wa Magharibi wa Fatick
  • Waziri mkuu wa zamani
  • Alipishana na Rais baada ya kumtaka Karim Wade ajibu maswali bungeni
  • Ni mgombea pekee wa upinzani kufanya kampeni kwa nchi nzima.

Kambi ya Bw Wade imesema Rais wa sasa ana uhakika wa ‘kushinda kwa kishindo’ katika duru ya kwanza.

Lakini Bw Sall anaamini anaamini kuwa "duru ya pili ni lazima, tumeshinda sehemu muhimu nchini."

Mtaalamu huyo wa madini mwenye umri wa miaka 51na meya wa mji wa magaharibi wa Fatick, anayewania kwa mara ya kwanza alionya pia kuhusu udanganyifu katika kura.

Mwandishi wa BBC Thomas Fessy mjiniDakaranasema Bw Sall amekuwa mgombea pekee wa upinzani anayeendesha kampeni makini nchi nzima huku wagombea wengine wakijihangaika kuwahamasisha watu kwenye mitaa yenye maandamano.

Iwapo dura ya pili imethibitishwa muungano wa "yeyote isipokuwa Wade" unaweza kuwa ushindi nyuma ya Bw Sall, mwandishi wa BBC anasema.

Mahakama ya Kikatiba yaSenegaliliamua Bw Wade anaweza kuwania tena kwa misingi kuwa awamu yake ya mwanzo haikuhesabiwa kwani ilianza kabla ukomo wa awamu mbili haujawekwa kisheria mwaka 2001.

Mahakama pia ilimzuia mwanamuziki mashuhuri duniani Youssou N'Dour kugombea katika uchaguzi huo.

Bw N'Dour alisema kuwa kumruhusu Bw Wade kuwania tena kunasebabisha mapinduzi ya kikatiba.

Senegal, koloni la zamani la Ufaransa, inaonekana kuwa thabiti kidemokrasia na mfululizo wa uchaguzi tangu uhuru mwaka 1960.

Inabakia nchi pekee ya Afrika Magharibi ambako jeshi halijachukua madaraka.