Wawili wauawa na maharamia wa Kisomali

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Moja ya chombo cha maharamia wa Kisomali

Mateka wawili wameuawa baada ya manowari ya jeshi la Uholanzi kujaribu kuokoa meli ya mizigo iliyotekwa na maharamia wa Kisomali.

Wanamaji wa Uholanzi wamesema walifyatulia risasi meli hiyo kujaribu kutibua utekaji nyara.

Manowari hiyo iitwayo Absalon imekuwa ikifuatilia meli iliyotekwa nyara siku chache zilizopita.

Wakati maharamia wakijaribu kuondoa meli waliyoiteka karibu na eneo la mwambao, wanamaji wa Uholanzi walifyatua risasi kama kuwaonya lakini maharamia wakaendelea kuamuru meli hiyo kuondoka.

Hii ililazimu manowari kufyatua risasi wakilenga injini ya meli iliyotekwa.

Katika tukio hilo maharamia wote 17 walijisalimisha.

Mabaharia wawili walijeruhiwa vibaya na walikufa kutokana na majeraha licha ya juhudi za dharura kuokoa maisha yao kutoka kwa daktari wa manowari hiyo.

Uchunguzi umeanzishwa kubaini mazingira yaliyosababisha vifo vya mabaharia hao.

Kongamano la hivi karibuni kuhusu Somalia lilijadili jinsi ya kuangamiza mitandao yote inayotumiwa kufadhili shughuli za uharamia pwani ya Somalia ambapo mamilioni ya dola zimelipwa kama kikombozi.