Meli ya watalii bahari Hindi yavutwa

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Costa Allegra meli ya kitalii iliyokwama bahari Hindi yavutwa

Meli ya watalii ya Kitaliana iliyokuwa ikipwelea katika bahari ya Hindi ikiwa na zaidi ya watu 1,000 baada ya kupotelewa na umeme imevutwa hadi kisiwa kimoja cha Ushelisheli.

Meli ya uvuvi ya Ufaransa inaivuta meli hiyo Costa Allegra hadi kwenye kisiwa hicho ambako inatazamiwa kuwasili siku ya Jumatano.

Moto uliotokea katika chumba chenye jenereta ya meli hiyo siku ya Jumatatu ulisababisha kupoteza nguvu zote za umeme.

Meli hiyo inatoka shirika moja na ile meli ya Costa Concordia, ambayo ilikwenda mrama nje ya mwambao wa Italia mwezi Januari ambapo watu 32 walipoteza maisha yao.

Mwaandishi wa BBC Katy Watson aliyeko Ushelisheli anasema meli hiyo inavutwa hadi kisiwa cha Desroches , karibu na kisiwa cha Alphonse kusini Magharibi mwa Ushelisheli.