Uganda kujenga kambi zaidi za wakimbizi

Uganda imepanga kuunda kambi mpya ili kukidhi idadi kubwa ya wakimbizi kutoka magharibi mwa Jamhuri ya Congo, kwa mujibu wa msemaji wa serikali.

Image caption Wakimbizi wa Congo

Waziri anayehusika na wakimbizi ameiambia BBC kua kwa uchache watu 100 wanaingia nchini Uganda kila siku wakikimbia ongezeko la ghasia.

Wanawake wamedai kua walibakwa na wapiganaji wa makundi ya mgambo waliowaingilia katika nyumba zao usiku na pia kuiba chakula na mali.

Hadi watu 3,000 wameikimbia Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo tangu uchaguzi wa mwezi Novemba uliozua utata.

Makundi kadhaa ya waasi bado yanaendelea na shughuli zao za uasi katika nchi ya Congo yenye utajiri mkubwa wa madini licha ya vita vya wenyewe kumalizika rasmi mnamo mwaka 2003.

Masuala ya Uchaguzi

Waziri wa masuala ya wakimbizi wa Uganda, Stephen Malinga, anasema kua kambi mpya ya wakimbizi inahitajika kwa sababu kambi zilizokuwepo za Nakivale na Oruchinga karibu na mji wa Mbarara zimezidiwa.

Kwa mda wa miaka mingi Makumi kwa maelfu ya raia wa Congo wamekua wakikimbia nchi yao na hivi sasa nchi hiyo inakabiliwa na jinsi ya kujikwamua kutoka mgogoro huo ambao umesababisha takriban vifo vya watu milioni tatu.

Mwandishi wa BBC Ignatius Bahizi alitembelea kambi ambako watu 6,000 wamewasili tangu mwezi julai. Wakimbizi waliowasili hivi karibuni walimfahamisha juu ya mauwaji utekaji nyara na ubakaji unaofanywa na watu wenye silaha.

Baadhi ya wakimbizi waliokimbia maeneo yaliyo karibu na mji wa Goma, Masisi na Rutshuru, walisema kua watu wenye silaha waliwahoji kuhusu jinsi walivyopiga kura nani walimpigia katika uchaguzi wa mwaka jana.

Uchaguzi huo, ukiwa wa kwanza kuandaliwa nchini Congo tangu kumalizika kwa vita, na kmshindi akawa Rais Joseph Kabila, lakini matokeo yakapingwa na kiongozi wa upinzani Etienne Tshisekedi.

Bw. Malinga, aliyetembelea wakimbizi hao wiki iliyopita anaamini kuongezeka kwa ghasia huenda kumesababishwa na masuala ya kisiasa au jinsi watu walivyopiga kura.