Kamati ya katiba yajadiliwa Misri

Kikao cha pamoja cha bunge la Misri kimeanza kujadili umbo la kamati ambayo itatunga katiba mpya, kuchukua nafasi ya katiba ya zamani iliyofutwa na jeshi baada ya Rais Hosni Mubarak kuondolwa madarakani mwaka uliopita.

Haki miliki ya picha AP

Vyama vya Waislamu vilivoshinda katika uchaguzi uliofanywa mwisho wa mwaka jana, vinasema kuwa vinafaa kuongoza katika kamati hiyo itayokuwa na wajumbe 100.

Waandishi wa habari wanasema vyama hivyo vitapingana na halmashauri ya kijeshi inayoongoza nchi sasa, ambayo inapenda heshima inayopata kwenye katiba ya sasa, na wanasiasa wa msimamo wa wastani, ambao wana wasiwasi kuwa hawatokuwa na kauli katika katiba mpya.

Ripoti zinasema kuwa orodha ya majina ya wajumbe wa kamati itatangazwa mwisho wa mwezi huu.