Uchina yazidisha bajeti ya jeshi

Wakuu wa Uchina wanasema watazidisha bajeti ya jeshi mwaka huu kwa zaidi ya asili-mia-10, na kufikia zaidi ya dola bilioni 100.

Haki miliki ya picha AP

Bajeti hiyo ya jeshi ndio ya kwanza kutangazwa tangu Rais Obama aliposema kuwa Marekani itazidisha nguvu zake katika eneo la Asia-Pacific.

Jeshi la Uchina linaweka mipango yake siri sana.

Wadadisi wanaamini kuwa bajeti hasa ni kubwa zaidi kushinda ile inayotajwa rasmi.

Uchina inasisitiza kuwa lengo la mradi wa kuimarisha zana zake za kijeshi ni la salama.

Lakini kila Uchina ikizidi kuwa na kauli katika bara la Asia, majirani zake nao wanazidi kuwa na wasi-wasi juu ya azma hasa ya taifa hilo.

Awali mwaka huu Marekani ilitangaza mkakati mpya wa kijeshi, ili kupambana na nguvu za Uchina zinazozizidi.

Marekani imetoa wito kuwa mataifa hayo mawili yashirikiane katika shughuli za kijeshi.

Bajeti rasmi ya jeshi ya Uchina ni ndogo sana ikilinganishwa na Marekani.

Lakini Uchina bado inatazama kwa makini madaraka ya Marekani yakiongezeka katika eneo hilo, na inaamini kuwa Marekani inataka kuizingira.