Congo-Brazzaville yaomba msaada wa dharura

Majeruhi wafurika hospitali Brazzaville Haki miliki ya picha AP

Maafisa wa Jamuhuri ya Congo wameomba msaada kwa jamii ya kimataifa baada ya kutokea mlipuko katika bohari la silaha na kuwaua watu 150 waliuawa, na wengine 1500 kujeruhiwa. Mlipuko huo ulitokea jiji kuu, Brazzaville na makundi ya wakozi yanaendelea kuwatafuta manusura.

Makaazi na majengo yaliporomoka baada ya bohari la silaha kulipuka na kuwaua makumi ya watu huku wengine wengi wakijeruhiwa. Wengi walihofia kutokea tetemeko la arthi au mapinduzi ya serikali katika nchi ambayo imewahi kukumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Hospitali zinakumbwa na wakati mgumu kukidhi idadi kubwa ya majeruhi. Chumba cha kuhifadhi maiti mjini Brazzaville kimepokea maiti 146 na kinaendelea kupokea maiti zaidi.

Maafisa wamesema bohari hilo linahifadhi silaha za vita yakiwemo makombora. Mlipuko huo ulitikisa eneo kubwa kiasi cha kusikika mji wa Kinshasa katika nchi jirano ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Serikali imelaumu hitilafu ya nyaya za umeme kwa kutokea mlipuko huo.Muungano wa Afrika umetuma rambirambi na kuitaka jamii ya kimataifa kusaidia Congo Brazzaville.Wizara ya mambo ya nje ya Ufaransa imetangaza kutuma mzaada wa dharura mjini Brazzaville.