Kofi Annan apinga jeshi Syria

Kofi Annan Haki miliki ya picha Getty

Aliyekua katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, ametoa wito wa kukomesha ghasia nchini Syria, mwanzoni mwa ziara yake ya kutafuta amani ya nchi hio.

Hata hivyo Kofi Annan amepinga vikali fikra yoyote ya ufumbuzi wa mgogoro wa Syria kupitia nguvu ya majeshi ya Kimataifa. Aliyasema wakati akiwa kwenye Makao makuu ya Jumuia ya nchi za Kiarabu mjini Cairo

Huu ulikua mwanzo wa wengi walichokitaja kama safari ngumu kwa Katibu huyo wa zamani wa Umoja wa Mataifa.

Akizungumza baada ya kikao cha mjini Cairo, Kofi Annan amesema kua anaungwa mkono na Jumuia ya Kimataifa katika juhudi hizi.

Alisema kua shabaha yake ni kukomesha ghasia nchini Syria, kufungua njia ya kuwezesha misaada ya kimataifa kuwafika wanaohitaji msaada na pia kuanzisha mchakato wa kisiasa ambao unaweza kufikia suluhu kwa wahusika wote.

Alipoulizwa kuhusu suluhu la kijeshi, Kofi Annan alijibu kwa kusema kua hakuna yeyote anayetafakari matumizi ya kijeshi. Hilo linaweza tu kuzidisha hatari, aliongzeae na kusema kua dawa hio inaweza kua na sumu zaidi ya maradhi.

Matamshi hayo yametofautiana na Seneta wa Marekani, John McCain, ambaye hivi karibuni aliitisha mashambulizi ya anga na maoni ya baadhi ya nchi za Kiarabu zinazotaka kuona waasi wa Syria wakipewa silaha.