Waziri wa Marekani matatani

Image caption Wapenzi wa jinsia moja Uganda

Shirika moja la kutetea haki za wapenzi wa jinsia moja limeshitaki waziri mmoja wa Marekani likimtuhumu kwa kuhusika na kampeini ya kuwakandamiza wapenzi wa jinsia moja nchini Uganda.

Hata hivyo waziri huyo Scott Lively, anakanusha madai ya kuyachochea makundi yanayopinga wapenzi wa jinsia moja kuwanyanyasa

Alifahamisha BBC kuwa kesi hiyo inahusu madai ambayo yametafsiriwa visivyo na hivyo akaitaka mahakama isichukue hatua zozote.

Shirika hilo, Sexual Ministries Uganda, linataka bwana Lively kuchukuliwa hatua kwa kile alichofanya nchini Uganda pamoja na kulipa fidia kwa kitendo chake.

Vuguvugu la ''Center for Constitutional Rights (CCR)'', liliwasilisha kesi hiyo mahakamani kwa niaba ya shirika la kutetea haki za wapenzi wa jinsia moja, ''Sexual Ministries Uganda'' katika mahakama moja katika jimbo la Massachusetts, Marekani ambako anaishi bwana Lively.

Kesi hiyo imewasilishwa mahakamani Marekani kulingana na sheria wanayosema inaruhusu raia wa kigeni kuwashtaki wamarekani wanaoshukiwa kukiuka sheria za kimataifa nchini humo.