Viongozi Afrika Magharibi kuelekea Mali

Haki miliki ya picha AP
Image caption Viongozi wa ECOWAS wakijadiliana jambo kuhusu Mali

Ujumbe wa viongozi wa nchi za Afrika Magharibi uko njiani kuwasili Mali kujadiliana na viongozi wa mapinduzi ambayo yalimwondoa madarakani Rais wiki iliyopita.

Viongozi kutoka Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi-ECOWAS wanafanya mazungumzo na kiongozi wa mapinduzi hayo Capt Amadou Sanogo.

Wameonya Mali kurejesha mara moja utawala wa kikatiba na wameweka majeshi ya kulinda amani katika hali ya tahadhari.

Jumatano maelfu ya watu waliingia mitaani katika mji mkuu Bamako kuwaunga mkono waliofanya mapinduzi.

Wengi walikarishwa na kile walichokiona kama ‘kuingiliwa na wageni’ nchini mwao.

"Viongozi wa mapinduzi wanatakiwa kutatua matatizo kaskazini,ufisadi na elimu. Hayo ni muhimu kuliko uchaguzi. " Mmoja wa waandamanaji, Khalifa Sogo, aliliambia shirika la habari la Reuters.

Katiba Mpya

Mwenyekiti wa Ecowas Rais wa Ivory Coast Alassane Ouattara, alisema demokrasia ya Mali haiwezi kuachwa ipotee.

"Hatuwezi kuruhusu nchi yenye demokrasia na vyombo vya kuisimamia ikaanza kurudi nyuma kwa miongo miwili iliyopita, na kuachia historia irudi nyuma," Alisema Bw Ouattara.

"Ni kwa misingi hiyo Mali inahitaji haraka kurudisha vyombo vya demokrasia katika hali ya kawaida." alisema.

Baadhi ya wachambuzi wanasema kuwepo kwa vikosi vya kulinda amani kunaonyesha kuwa chombo hicho kinaweza kutumia nguvu iwapo Kepteni Sanogo hatakubali kuondoka madarakani.

Viongozi wa mapinduzi wametoa maelezo ya katiba mpya pamoja na kutangaza tarehe ya uchaguzi ambapo wale waliohusika na mapinduzi hawataruhusiwa kushiriki ingawa tarehe halisi haijatangazwa bado.

Mapinduzi yaliongozwa na askari ambao hawakufurahishwa na jinsi serikali ya Bw Toure ilivyokuwa ikishughulikia suala la waasi wa Tuareg kaskazini mwa nchi.

Waasi wa Tuareg waliviondoa vikosi vya jeshi katika miji kadhaa ya kaskazini katika miezi ya hivi karibuni.

Chini ya katiba mpya kamati ya mpito yenye wajumbe 26 kutoka vikosi vya usalama na raia 15 watashirika madaraka.

Wale watakaofanya kazi katika kamati hiyo wamepewa kinga ya kushtakiwa.

Baadhi ya nyaraka katika katiba hiyo zinafanana na katiba ya sasa ya Mali zikiwemo uhuru wa kujieleza, wa mawazo na kutembea.

Rais aliyeondolewa madarakani Amadou Toumani Toure alisema Jumatano kuwa ataendelea kubaki nchini, yuko huru na mwenye afya njema.

"Nadhani kitu muhimu leo ni kuwa tunahitaji maelewano kupata suluhu ya mgogoro huu. Kitu cha muhimu hapa si ATT, sio mtu. Kile cha muhimu ni demokrasia, na taasisi zetu,Mali." Alikiambia kituo cha Radio ya Ufaransa RF1.