Rais wa Mali kushtakiwa kwa uhaini

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Majeshi yaliyopindua serikali Mali

Watawala wa kijeshi wanapanga kumfungulia mashtaka ya uhaini rais waliyempindua. Kiongozi wa Mapinduzi Kapten Amadou Sanogo amesema pamoja na mashtaka mengine, Amadou Toumani Toure anakabiliwa na ubadhirifu wa fedha za umma.

Haya yanajiri wakati watawala wa kijeshi wametangaza kuanza kongamano la kitaifa kujadili mustakabali wa Mali. Nchi hiyo ambayo haina bandari imewekewa vikwazo vya kiuchumi na jamii ya kimataifa.

Wanajeshi wa daraja ya chini waliipindua serikali kutokana na kile walisema mikakati duni ya kukabiliana na waasi kaskazini mwa nchi. Tangu mapinduzi hayo , nao waasi wameendelea kuyateka maeneo mengi kaskazini mwa Mali ukiwemo mji wa Timbuktu ambao una hifadhi maalum za kitamaduni.

Waasi hao wamegawanyika makundi mawili ambapo lile la MNLA linapigania kuwepo taifa huru la Azawad. Kundi nyingine Ansar Dine lenye uhusiano na mtandao wa Al-Qaeda linataka kusalia Mali lakini chini ya sheria ya Kiisilamu.

Rais Amadou Toumani Toure alitarajiwa kuondoka madarakani baada ya kumaliza muhula wake wa pili baadaye mwezi huu.Wakati huo huo Waasi hao wa Kaskazini wameendelea kusonga hatua mbele kusini mwa Mali.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kutoa taarifa kuhusu mzozo wa Mali baadaye Jumatano wiki hii.