Kundi la jeshi la asi huko DRC

Image caption Bosco Ntaganda

Mamia ya wanajeshi wameasi jeshi la Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Duru za kibalozi zimesema wanajeshi watiifu kwa aliyekuwa kiongozi wa waasi Bosco Ntaganda walianza kuondoka jeshini mapema wiki hii.

Ntaganda anatakiwa na mahakama ya kimataifa- ICC kwa kutekeleza dhuluma za vita.Wasi wasi umetanda mjini Goma Mashariki mwa DRC ambapo ni ngome kuu ya Ntaganda.

Wiki jana Ubeljiji ilitaka serikali ya Congo kumkamata Bosco Ntaganda na kumkabidhi kwa ICC. Kamanda huyo wa jeshi ameshtakiwa kwa kuwasajili watoto jeshini, mauaji na ubakaji.

Katika ziara yake mjini Kinshasa, Waziri wa Mambo ya nje wa Ubeljiji Didier Reynders alimuelezea rais Joseph Kabila kwamba sifa ya serikali yake inapata doa kwa kushindwa kumkabidhi Bosco Ntaganda kwa ICC.

Mhariri wa BBC wa masuala ya Afrika Martin Plaut amesema hatua ya majeshi tiifu kwa Ntaganda kuasi jeshi la taifa ni onyo kuwa watajibu jaribio lolote kumkamata kamanda wao Bosco Ntaganda.