Waasi wa Tuareg wakomesha harakati

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Waasi wa Tuareg

Waasi wa Tuareg nchini Mali, wametangaza kusitisha harakati zao za kijeshi nchini humo.

Kulingana na taarifa kwenye mtandao wa waasi hao , kundi hilo la ukombozi wa eneo la Azawad, (MNLA) limeteka maeneo ya kutosha kuweza kuunda jimbo lao wenyewe.

Lakini kundi la wapiganaji wa kiisilamu waliosaidiana na waasi wa Tuaraeg kupigania maeneo hayo, halijatoa masimamo wake.

Viongozi wa majeshi ya nchi za magharibi, wanatarajiwa kukutana kujadili namna watakavyo shurutisha viongozi wa mapinduzi Mali kuondoka mamlakani.

Kundi la wanajeshi wengi walipindua serikali mwezi jana, wakidai kuwa serikali ya kiraia haikukabiliana vilivyo na waasi wa Tuareg.

Lakini MNLA pamoja na wapiganaji wa kiisilamu, Ansar Dine, inaarifiwa walipata fursa ya kusonga na kuvamia eneo la Kakazini mwa Mali, punde baada ya jeshi kupindua serikali.

Kwingineko, mkutano wa kisiasa ulioitishwa na wanajeshi waasi, kujadili namna ya kukabidhi mamlaka ya kiraia, hii leo, ilifutiliwa mbali, baada ya vyama vyote vya kisiasa kukataa kuhudhuria.

Mnamo Jumatano, baraza la usalama la umoja wa mataifa, lilitoa azimio la kutaka mapigano kukomeshwa nchini Mali, ombi lililoitikiwa na waasi wa MNLA, wakitangaza rasmi kusitisha harakati zao.