Mutharika asafirishwa Afrika Kusini

Rais Bingu wa Mutharika kwa wakati huu amepoteza fahamu kufuatia mshituko wa moyo.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Mutharika apelekwa Afrika Kusini kwa matibabu

Kutokana na hali hiyo,Mutharika amesafirishwa hadi Afrika Kusini kwa matibabu zaidi na

aliondoka katika uwanja wa ndege wa Lilongwe milango ya saa sita na nusu usiku kuelekea Johannesbuerg.

Alisafirishwa Afrika kusini katika hali ya usiri mkubwa na akiwa hana fahamu.

Walioandamana nae ni mkewe na jamaa wa karibu zaidi wa rais huyo

Hii imezuia hali ya hofu na utata mkubwa nchini Malawi kwani kwa muda mrefu kumekuwa na shinikizo za kumtaka Mutharika ang’atuke .

Radio ya kitaifa ilikuwa imetangaza kuwa kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 78 na ambaye alikuwa hali mahututi atapelekwa hadi afrika kusini kwa matibabu maalum.

Wakati huo huo viongozi wa Malawi walitaka nchi iwe na utulivu huku watu wakimuombea apate afueni.

Afisa mmoja mkuu wa serikali ya Malawi alinukuliwa akisema kuwa Rais Mutharika aliangua akiwa katika makaazi yake rasmi na kupelekwa hospitalini ambako aliwekwa katika chumba cha wagonjwa mahututi.

Akiwa hospitalini chini Malawi, Mutharika alitembelewa na maafisa wakuu katika serikali yake wakiwemo mawaziri, mkewe na wanawe.

Makamu wa Rais Bi Jocye Banda alikuwa wakwanza kuthibitisha habari za kuugua kwa Mutharika.

Kabla ya tamko hilo Bi Banda vyombo vyote vya habari vilikuwa vimebana kutoa habari zozote kuhus hali ya raia Bingu wa Mutharika.

Lakini baada ya Makamu wa rais kufichua kuwa Kiongozi wao ni mgonjwa, ndipo Radio ya kitaifa ikatangaza kuwa Mutharika atapelekwa Afrika kusini kwa matibabu maalum.

Kulingana na katiba ya Malawi ikiwa Mutharika atashindwa kuendelea na kazi yake ya Urais basi Makamu wake Bi Joyce Banda atalazimika kushikilia hatamu za uongozi kwa kipindi kilichosalia .

Hata hivyo Bi banda na rais Mutharika walikuwa hawasikilizani kwani walikosana mwaka wa 2009 na Makamu huyo wa Rais akalazimika kuhamia upinzani.