Tuareg wajitangazia uhuru

Image caption Waasi wa Tuareg

Waasi walioteka Kaskazini mwa Mali wamejitangazia uhuru wao wa jimbo la Azawad, baada ya kudhibiti eneo hilo mwezi jana. Kundi la National Movement for the Liberation of Azawad (MNLA) limetoa taarifa ya uhuru wake kupitia wavuti wake na kusema litaheshimu mipaka ya nchi.

Kundi hilo ni moja wapo ya makundi mawili ambayo yanadhibiti kaskazini mwa nchi. Mali inakumbwa na msukosuko wa uwongozi hususan baada ya serikali ya kiraia kupinduliwa na jeshi. Wanajeshi hao wamelalamikia jinsi serikali ilivyoshughulikia maasi kaskazini mwa nchi.

Tangazo la uhuru wa Azawad linajiri wakati shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu Amnesty International limeonya kuzuka janga la kibinadamu kutokana na maasi ya Kaskazini.Mashirika ya misaada yameomba kukubaliwa kuingia maeneo yaliyotekwa kutoa misaada ya kibinadamu hasa baada ya uporaji uliofanywa maeneo ya gao, Kidal na mji wa kale wa Timbuktu.

Kundi la MNLA liliundwa mwaka jana na wapiganaji wa Ki-Tuareg ambao walimsaidia Kiongozi wa zamani wa Libya Kanali Muammar Gaddafi kuzima maandamano dhidi yake.

Umoja wa Mataifa umeelezea wasi wasi wake dhidi ya kundi jingine la Ansar Dine lenye uhusiano na mtandao wa Al-Qaeda na ambalo linaunga mkono kuwepo sheria ya dini ya kiisilamu nchini Mali.