Majonzi ya Kanumba

Kanumba Haki miliki ya picha blogs
Image caption Steve Kanumba alipata umaarufu mkubwa Afrika

Tanzania inaomboleza kifo cha Msanii maarufu wa Filamu nchini Tanzania Steven Kanumba aliyefariki Jumamosi jijini Dar es Salaam,

Tasnia ya filamu nchini Tanzania inaendela kuomboleza kifo cha msanii huyo maarufu wa filamu nchini humo ambaye amefariki usiku wa kuamkia Jumamosi nyumbani kwake Sinza Vatican jijini Dar es Salaam.

Taarifa zilizothibitishwa na mmoja wa ndugu za Marehemu, zinasema kuwa Marehemu Steven Kanumba alifariki majira ya saa nane usiku, muda mfupi baada ya kutokea mzozo kati yake yake na rafiki yake wa kike ambaye ni msanii mwenzake wa filamu.

Polisi mkoani Dar es Salaam imethibitisha kuwa inamshikilia kwa mahojiano msanii huyo wa kike kuhusiana na kifo cha Kanumba, ambaye alijizolea umaarufu mkubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na kati na hadi Afrika Magharibi baada ya kuwashirikisha katika filamu zake baadhi ya wasanii Maarufu wa Kinigeria akiwemo Mercy Johnson na Noah Ramsey.

Marehemu ambaye alizaliwa mwaka 1984, alianza kujipatia umaarufu mwanzoni mwa mwaka 2000 wakati huo akiigiza katika Michezo ya luninga kupitia kundi la maigizo la Kaole Sanaa.

Aliendelea na kuigiza filamu nyingi ambazo zilimpatia umaarufu mkubwa kiasi cha kusafiri mara kadhaa nchi za nje, ambako alitambulika kama mmoja wa wasanii wenye vipaji vikubwa ambaye aliitangaza fani ya filamu nchini Tanzania maarufu kama Bongo Movies.

Tangu kuanza kutangazwa kwa taarifa za kifo chake mapema alfajiri, mamia kwa maelfu ya watu wamekuwa wakimiminika kwa wingi nyumbani kwa marehemu, huku vyombo vingi vya habari vikizipa kipaumbele mara kwa mara taarifa za kifo cha msanii huyo.