Mshukiwa wa ugaidi kupelekwa Marekani

Haki miliki ya picha PA
Image caption Abu Hamza akizungumza na waislamu mjini London, atakiwa kusafirishwa Marekani

Mahakama ya Haki za Binadamu ya Ulaya imeunga mkono kusafirishwa kwa Abu Hamza na washukiwa wengine wanne wa ugaidi kutoka Uingereza hadi Marekani.

Mahakama ya Strasbourg imesema hakutakuwa na ukiukwaji wa haki za binadamu kwa wale wanaotumikia kifungo cha maisha jela.

Majaji wamesema watazingatia suala la mshukiwa mwingine kwa sababu ya maradhi ya akili.

Waziri Mkuu David Cameron amesema "ameridhishwa" na taarifa hizo.

"Ni vyema kwamba tuna mfumo mzuri wa sheria, ingawa wakati mwingine unaweza kufadhaishwa na muda ambao masuala haya yanavyoshughulikiwa," aliongeza.

Uamuzi huu wa mahakama ni muhimu sana tangu kutokea kwa mashambulio ya 9/11 kwa sababu unaunga mkono haki za binadamu kuzingatiwa katika magereza ya Marekani, na kufanya kuwa rahisi kwa Uingereza kuwapeleka washukiwa kwa washirika wake wa karibu.

Kimsingi kuna nafasi ya kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo wa mahakama - lakini kwa uzoefu, ni kesi chache ambazo huwa zinaangaliwa upya katika hatua hii.

Wanaume hao wana muda wa miezi mitatu kushawishi mahakama kuanzisha upya kesi hiyo. Kama watashindwa kukata rufaa, watasafirishwa hadi Marekani.

Familia ya mmoja wa washukiwa, Babar Ahmad, ambaye amekuwa akizuiliwa kwa miaka karibu nane bila kushtakiwa, wanasema wataendelea na mchakato wa kukata rufaa dhidi ya kusafirishwa Marekani.

Wiki iliopita, katika mahojiano na BBC aliomba kesi yake ifanyike Uingereza kwa sababu madai yanayomkabili yalitelekezwa nchini Uingereza.