Syria yachukua hatua kusitisha mapigano

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mjumbe wa amani wa UN kuhusu Syria Koffi Annan

Hali ya kusitisha mapigano imeanza kutekelezwa nchini Syria licha ya kuwa nchi za Magharibi zinatilia shaka nia ya serikali kutekeleza mapatano hayo.

Waandishi wa habari wanasema inaelekea kuwa pande zote zimesitisha harakati zao hakuna ripoti za maafa au vifo hadi sasa.

Hata hivyo kulikuwa na taarifa kadhaa za kufyatuliwa mizinga na risasi mapema asubuhi na vikosi vya kijeshi bado vipo mitaani.

Serikali ya Syria pamoja na vikundi vya wapiganaji wa upinzani wanasema watatekeleza mapatano hayo ya kusitisha mapigano,lakini watajibu mapigo iwapo wakishambuliwa..

Nchi jirani ya Uturuki imesema itafurahi sana ikiwa mpango wa Annan utafanikiwa.

Lakini Waziri wa Mambo ya nje wa Uturuki Ahmet Davutoglu ameaiambia BBC kwamba ikiwa amani itasambaratika na jamii ya kimataifa haitachukua hatua zozote,au kukiwa na tishio kwa usalama wa Uturuki basi itakuwa na haki ya kulinda mipaka yake na kuwasaidia watu wanaokimbia mauaji.

Uturuki imewapatia hifadhi zaidi ya wakimbizi 24,000 kutoka Syria na matukio ya ufyatuaji risasi katika eneo la mpaka yamesababisha watu sita kujeruhiwa katika upande wa mpaka wa Uturuki.

Waziri wa mambo ya nje wa Syria Jihad Makdissi ameaiambia BBC kuwa serikali imejitolea kwa dhati kusitisha harakati zote za kijeshi ikiwa hakutakuwa na hujuma zozote za kivita dhidi ya taifa.

"ikiwa hao wapinzani walioko nga'mbo wanataka kufurahia matunda ya nchi yao,lazima waje kwenye meza ya mazungumzo na majadiliano. "

Wizara hiyo pia imemuandikia mjumbe wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa nchi za Kiarabu , Kofi Annan - ambae ndiye aliyependekeza mpango huo -ikiahidi kuutekeleza lakini wakiwa na haki ya kujibiza mashambulio yoyote ya waasi.

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Susan Rice alielezea masharti hayo kama yenye kuzusha wasiwasi na kusema jukumu ni la utawala wa Syria kusitisha utumiaji nguvu.

Kanali Kassem Saadeddine, kutoka mojawapo wa vikundi vikuu vya waasi,Jeshi huru la Syria , alisema "ikiwa utawala huo hautasimamisha mashambulio ya mizinga na kuondoa vifaru basi tutaongeza harakati zetu na kuanzisha mashambulio".