Roketi ya Korea Kaskazini yaanguka

Habari kutoka Japan, Korea Kusini na Marekani zinasema kuwa mpango wa Korea Kaskazini wa kurusha angani roketi umeshindwa.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mtazamaji aangalia katika runinga kurushwa kwa Roketi ya Korea Kaskazini

Roketi hiyo ilitazamiwa kupaa angani katika hatua tatu, kuelekea Kusini kutoka eneo ilikorushiwa, kupitia ufuo wa Magharibi wa Korea na kupita katikati mwa kisiwa kilichoko katikati mwa Taiwan na Japan cha Okinawa, kabla ya kuanza sehemu yake ya pili ya kupaa angani karibu na Ufilipino.

Lakini vyombo vya habari vya Marekani vinasema kuwa kulikuwa na mwanga mkubwa zaidi baada ya roketi hiyo kuwa sekunde 90 angani, na msemaji wa jeshi la Korea Kusini alisema kuwa urushaji huo wa roketi umefeli.

Alifafanua kwamba kombora hilo lilikatika vipande viwili na kuanguka chini.

Licha ya kutofualu kwa urushaji huo wa roketi angani ni wazi kuwa watu wengi watashutumu jaribio hilo.

Baraza la Usalama la umoja wa Mataifa limetangaza kuwa litakuwa na kikao maalumu hii leo na Rais wa Korea Kusini amesema kuwa maafisa wakuu wa usalama wataandaa kikao maaulu cha kujadili usalama nchini.