Guinea Bissau yaonywa kufuata katiba

Jumuia ya nchi zinazotumia Kireno imependekeza kuingilia kati kijeshi nchini Guinea Bissau baada ya mapinduzi ya Alkhamisi, ambapo rais na waziri mkuu walikamatwa.

Haki miliki ya picha INTERNET

Katika mkutano uliofanywa mjini Lisbon, uliohudhuriwa na waziri wa mashauri ya nchi za nje wa Guinea-Bissau, nchi nane za jumuia zilitishia kuiwekea Guinea Bissau vikwazo iwapo katiba haitafuatwa.

Jumuia ya nchi zinazotumia Kireno, CPLP, ililaani mapinduzi yaliyofanywa Alhamisi, na kutaka maafisa wa serikali wafunguliwe bila ya kudhuriwa.

Taarifa iliyotolewa na jumuia hiyo ya nchi nane, imeahidi jumuia itashirikiana na mashirika ya Afrika na Umoja wa Ulaya, kumaliza msukosuko wa Guinea-Bissau kwa salama.

Lakini piya ilisema ina azma ya kuunda kikosi cha kuingilia kati, kitachopata idhini ya Umoja wa Mataifa, ili kuhakikisha kuwa katiba inafuatwa.

Duru ya pili ya uchaguzi wa rais, ambayo imevunjwa kwa sababu ya mapinduzi, lazima ifanywe, jumuia ya CPLP ilisema.

CPLP piya imesifu ile ilichosema mchango muhimu wa kikosi kidogo cha Angola kilioko Guinea-Bissau, ambacho kilileta mvutano jeshini.

Wanajeshi 200 wa Angola walipelekwa kuisaidia serikali ya Guinea Bissau kubadilisha jeshi lake, ambalo lina tabia ya kuingilia kati ya siasa za nchi.

Waangola wakitarajiwa kuondoka karibuni.