Wanajeshi Mali wazuilia wanasiasa

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Wanajeshi wa Mali

Wanajeshi nchini Mali wamemkamata Waziri Mkuu wa zamani na mwanasiasa mwenzake siku chache baada ya kurejesha utawala wa kiraia kufuatia mapinduzi ya mwezi jana.

Mmoja wa wasaidizi wa Modibo Sidibe amesema mwanasiasa huyo amechukuliwa na watu waliovalia sare za jeshi. Soumaila Cisse mmoja wa wagombea wakuu katika uchaguzi ujao pia anazuiliwa.

Mwandishi wa BBC Martin Vogl anasema tukio la sasa ni dalili kwamba kiongozi wa mpito hana madaraka kamili. Bw.Sidibe alikamatwa saa chache baada ya mapinduzi kabla ya kuachiwa huru.

Mali inajaribu kuweka taasisi imara za uwongozi kabla ya taifa hilo kuandaa uchaguzi wa urais.Muungano wa ECOWAS, Marekani na Muungano wa Ulaya zimetaka wanajeshi kujiondoa siasa na kurejea kambi zao mara moja.

Vikwazo vilivyowekewa Mali na ECOWAS viliwashawishi watawala wa kijeshi kurejesha utawala wa raia ambapo Dioncounda Traore aliteuliwa kaimu rais kusaidia mipango ya kuandaa uchaguzi, pamoja na kuzima maasi kaskazini mwa nchi.

Tangu kutokea Mapinduzi, waasi wa Tuareg na wapiganaji wa kiisilamu wameidhibiti maeneo mengi ya kaskazini ambayo ni jangwa.