Sudan, S. Kusini zazusha wasiwasi zaidi

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wanajeshi , ishara ya mapigano

Sudan Sudan Kusini zimeshutumiana kwa kufungua eneo jipya la mpaka wa mapigano katika eneo linalogombewa na kuongeza wasiwasi wa kuzuka vita.

Mapigano yalianza kaskazini mwa Aweil Sudan Kusini kiasi cha maili 100 (160 kilometa) magharibi mwa Heglig eneo lenye mafuta, chanzo cha mapigano ya sasa.

Askari saba wa Sudan Kusini na raia 15 waliuawa, msemaji wa jeshi la Sudan Kusini aliiambia BBC.

Sudan Kusini ilijitenga mwaka jana lakini mpaka wake na Jamhuri ya Sudan haujafikiwa makubaliano.

Jumanne wajumbe waliliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa Sudan na Sudan Kusini sasa ‘zimejifungia kwenye kongwa la vita.’

'mtazamo wa kivita'

Mapigano ya hivi karibuni yamechochewa na kuuawa kwa kupigwa risasi askari wa Sudan Kusini aliyekwenda kuchota maji Jumanne usiku, msemaji wa jeshi la Sudan Kusini Kanali Philip Aguer alisema.

Ilitokea katika barabara kati ya Aweil na Meiram katika jimbo la Darfur nchini Sudan katika kijiji kinachojulikana na wasudan Kusini kama Agok na watu wa Khartoum kama kambi ya Bahr al-Arab.

Sudan haijasema chochote lakini Kanali Fathi Abdalla Arabi, meya wa Meiram, amethibitisha mapigano hayo kupitia kituo cha mtandao wa vyombo vya habari vyaSudan, ambao una uhusiano wa karibu na serikali.

Mapigano ya karibuni kabisa yamejikita Heglig, eneo lililokaliwa na Sudan Kusini wiki iliyopita na yakasambaa zaidi katika mpaka na kusababisha wasiwasi mkubwa, anasema mwandishi wa BBC James Copnall akiwa Khartoum.

Sudan Kusini ilipata uhuru wake baada ya miongo miwili ya vita na Kaskazini na sasa inaendeshwa na harakati za waasi wa zamani.

Historia ngumu kati ya nchi hizo mbili haiwezi kudharauliwa, na inaweza kuthibitisha ugumu wa nchi zote kuondoka katika mtazamo wa kivita, mwandishi wa BBC anasema.