Uchaguzi G. Bissau kuchelewa

Haki miliki ya picha INTERNET
Image caption Wanjeshi wa Guinea Bissau

Watawala wa kijeshi nchini Guinea-Bissau wamesema uchaguzi wa urais utafanyika baada ya miaka miwili kufuatia mapinduzi ya wiki jana.

Waandishi wa habari wanasema msimamo huu hautaridhiwa na jamii ya kimataifa pamoja na wapatanishi kutoka kanda ya ECOWAS.

Guinea Bissau imesimamishwa uwanachama wa Muungano wa Afrika hadi pale wanamapinduzi watakaporejesha utawala wa kiraia.

Wakati huo huo Benki ya dunia na Benki ya maendeleo Afrika zimesimamisha ufadhili wa miradi ya ustawi katika nchi hiyo.

Guinea-Bissau ina historia ya mapinduzi ya kijeshi tangu kupata uhuru wake mwaka wa 1974.

Nchi hii ya Afrika Magharibi ni moja wapo ya masikini zaidi duniani huku asilimia 70 ya raia wake wakiishi kwa umasikini mkubwa. Ni taifa ambalo hutegemea zaidi msaada kutoka nje.

Mapema wiki hii wapatanishi kutoka kanda ya Afrika Magharibi ECOWAS walifanya mazungumzo na watawala wa kijeshi na kusema wameridhia kuyakabidhi madaraka kwa raia.

Wanajeshi wametetea hatua ya kufanya mapinduzi ambapo amepinga mpango wa serikali kupunguza idadi yao.

Rais wa mpito Raimundo Pereira pamoja na Waziri Mkuu Carlos Gomes Junior walikamatwa na wanajeshi hao wakati wakifanya mapinduzi.

Hakuna kiongozi wa Guinea Bissau anayemaliza mhula wake madarakani kabla ya kupinduliwa.Nchi hiyo pia imeoridheshwa kama kivukishio salama cha mihadarati kutoka Amerika Kusini hadi Bara Ulaya.