Rais Obama ataka mapatano Sudan

Rais Obama ametoa wito kuwa mapigano baina ya Sudan Kaskazini na Kusini yamalizwe, na marais wa nchi zote mbili wawe na ujasiri wa kutatua tofauti zao kwa amani.

Haki miliki ya picha BBC World Service

Bwana Obama alisema Sudan Kaskazini inafaa kusitisha hatua za kijeshi dhidi ya jirani yake pamoja na mashambulio ya ndege; na Sudan Kusini iache kusaidia makundi yenye silaha ndani ya Sudan Kaskazini, na harakati zake za kijeshi mpakani.

Baada ya Sudan Kusini kuviteka visima vya mafuta kwenye eneo la Heglig la mpakani siku kumi zilizopita, nchi hizo zilikaribia vita, lakini majeshi yake yameondoka, baada ya malalamiko ya kimataifa.

Hapo awali, Rais Omar al-Bashir, aliyasifu majeshi ya Sudan Kasakzini kwa kuwatimua wanajeshi wa Sudan Kusini huko Heglig.

Lakini mwakilishi wa Sudan Kusini katika Umoja wa Mataifa, Agnes Oswaha, alisema wanajeshi wao wanaondoka kama ishara kuwa nchi yake inataka amani.