Grand Prix yasonga mbele Bahrain

Mashindano ya magari ya langa-langa ya Formula One Grand Prix, yameanza Bahrain ingawa upinzani umetoa wito kuwa resi hizo zivunjwe.

Haki miliki ya picha AFP

Wakuu wa Bahrain wanasema wanaamini mashindano hayo hayataharibiwa na maandamano.

Kando ya barabara ambapo magari yatapita, kuna usalama mkubwa.

Wakuu wamevinjari kuwatenga waandamanaji mbali na njia ya mashindano, ambako wamewekwa askari wengi.

Mashindano hayo ni tukio kubwa la kimataifa kwa nchi ndogo kama Bahrain inayoongozwa na mfalme ...tukio ambalo likitarajiwa kuonesha nchi imerudi katika hali ya utulivu baada ya ghasia za mwaka jana.

Lakini badala yake matatizo ya nchi ndio yamejitokeza wazi kwa ulimwengu mzima, huku upinzani ukitumia fursa hii kuonesha malalamiko yao, wakati macho ya ulimwengu yako juu ya nchi yao.

Kifo cha muandamanaji mmoja - ambae mwili wake ulikutikana juu ya paa - kilizidisha mvutano kisiwani na kuzusha mapambano zaidi.

Mkesha wa mashindano, Waziri wa Mashauri ya Nchi za Nje wa Uingereza, William Hague, alizungumza na mwenzake wa Bahrain, akiwasihi wakuu wa Bahrain kuonesha uvumilivu kwa waandamanaji, na wasonge mbele kuleta mabadiliko nchini.