Mali yateua baraza la Mawaziri

Cheikh Modibo Keita Haki miliki ya picha AFP
Image caption Cheikh Modibo Keita

Rais wa serikali ya mpito wa Mali ametangaza serikali mpya,kwa kuwapa madaraka wanajeshi.

Wawakilishi wa majeshi wamepewa nyadhifa za Wizara ya Ulinzi, Wizara ya usalama wa nchini na masuala ya nchini.

Askari waliipindua serikali iliyochaguliwa kwa njia ya kidemokrasi takriban mwezi mmoja uliopita.

Viongozi wa mapinduzi hayo baadaye waliamua kukabidhi madaraka kwa Rais wa mpito Diouncounda Traore, aliyewajibishwa kuona kua ratiba ya uchaguzi inapangwa na kutekelezwa.

Mpango huu ulifikiwa na Shirikisho la kimkoa la Ecowas ambalo lilitaka kuhakikisha kwamba madaraka yarejeshwe kwa serikali itakayochaguliwa kwa kura.

Lakini kiongozi wa utawala wa majeshi, Capt Amadou Sanogo, amesisitiza kua kamati yake itaendelea kushiriki kama msimamizi hadi pale uchaguzi utakapofanyika. Mwandishi anayeishi mjini Bamako Martin Vogl ameiambia BBC.

Bw.Traore na Waziri wake mkuu, Cheick Modibo Diarra, wameliteuwa baraza la Mawaziri 24 kwa ujumla lakini hakuna miongoni mwao aliyekua katika serikali iliyopita.

Haifahamiki watahudumu kwa mda gani au Uchaguzi utafanywa lini.

Chagizo kuu kwa serikali ni kutenzua mgogoro ulioko kaskazini mwa nchi ambako Wa Tuareg pamoja na Waasi wanaofuata imani ya kiislamu wameteka eneo kubwa lenye ukubwa kuliko nchi ya Ufaransa.

Askari wa vikosi vya Mali walioshiriki mapinduzi ya serikali wamesema kua walilazimika kufanya hivyo kwa sababu serikali ilikua dhaifu katika kukabiliana na Watuareg.

Lakini wakati kukiwepo na pengo la uongozi uliopelekea waasi kuteka eneo wanaoliita Azawad.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Amadou Toure alikimbilia Senegal

Kiongozi wa zamani wa Mali aliyepinduliwa katika mapinduzi ya serikali, Amadou Toumani Toure, baadaye alikimbilia katika nchi jirani ya Senegal pamoja na familia yake.

Bw.Toure alisifiwa kwa kukomesha miaka mingi ya utawala wa kijeshi na kukabidhi madaraka kwa raia baada ya kuandaa uchaguzi wa mwaka 1992. Baadaye alichaguliwa kuongoza nchi.