Jeshi Uganda: 'kony anasaidiwa na Sudan'

Imebadilishwa: 30 Aprili, 2012 - Saa 12:42 GMT

Joseph Kony, Uganda yasema anasaidiwa na Sudan.

Jeshi la Uganda linasema kundi la waasi wa Lord's Resistance Army (LRA) linaloongozwa na Joseph Kony limekuwa linapata msaada kutoka kwa serikali ya Sudan.

Kundi la LRA linatuhumiwa kwa ubakaji, kukata watu viungo, kuwatesa, mauaji na kuwasajili watoto kuwa askari.

Kanali mmoja wa jeshi la Uganda ameiambia BBC wamemkamata mfuasi wa LRA aliyekuwa amevaa sare za Jeshi la Sudan na akiwa amebeba silaha na risasi.

Marekani imetuma kikosi maalum kusaidia kumsaka Konyi.

Ujumbe huo wa askari 100 unafanya kazi katika ngome nne nchini kote Afrika ya Kati ambako LRA linazunguka katika makundi madogo madogo likiiba mifugo na kuteka wanavijiji na kuwafanya wapiganaji, watumwa wa ngono ama wabeba mizigo.

Video iliyotolewa na kundi la uhamasishaji dhidi ya Kony kutoka Marekani la Invisible Children mapema mwaka huu lilisaidia kuamsha uelewa kwa jumuiya ya kimataifa kuhusu madhila yanayosababishwa na kundi hilo la LRA.

Mwezi uliopita Umoja wa Afrika ulitoa vikosi vya askari wapatao 5, 000 kumsaka mkimbizi huyo wa kivita.

Kony na wasaidizi wake wa karibu wamekuwa wakitafutwa kwa uhalifu wa kivita na mahakama ya Kimaifa ya ICC tangu mwaka 2005.

Hofu ya Kony ni halisi

Msemaji wa jeshi la Uganda Kanali Felix Kulayigye ameambia BBC kuwa jeshi hilo lina taarifa kuwa LRA sasa linasogea kuelekea Sudan, yakiwemo maeneo ya Darfur yanayodhibitiwa na wapiganaji wanaoungwa mkono na serikali wa Janjaweed.

"Kony anafahamu hatuwezi kuingia huko, kwa hiyo wakati shinikizo ni kubwa Afrika ya kati anavuka mpaka na kuingia maeneo ya Sudan," alisema.

Vikosi vya Marekani vinasaidia kumsaka Kony

Wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe ya Sudan kwa miongo miwili,Uganda iliwasaidia waasi, ambao mwaka jana waliongoza Sudan Kusini kupata uhuru wake, wakati serikali ya Sudan ilikuwa ikiaminiwa kuwasaidia waasi wa LRA ili kudhoofisha uwezo wa jeshi la Uganda.

Kamanda mwandamizi wa jeshi la Uganda hivi karibuni alisema nchi yake inaweza kuingilia kati mzozo wa Sudan na Sudan Kusini iwapo ungeendelea kuwa vita kamili, akimaanisha kuwa itaisaidia Sudan Kusini.

Kony, ambaye kikosi chake kiliinuka kwa mara ya kwanza kaskazini mwa Uganda ameponea chupuchupu kukamatwa kwa zaidi ya miaka 20 wakati vikosi vyake vikiendesha ugaidi katika maeneo ya Afrika ya Kati.

Anadai amekuwa akipigana kuiweka serikali yenye kufuata amri kumi za Biblia madarakani nchini Uganda.

Bw Kony alikuwa asaini mkataba wa amani na serikali ya Uganda mwaka 2008, lakini mazungumzo ya amani yalishindikana kwa sababu kiongozi wao alitaka uhakika kuwa yeye na wanaomuunga mkono hawatashtakiwa.

Mwandishi wa BBC Dan Damon ni miongoni mwa waandishi wa Habari waliotembelea ngome ya vikosi vya Marekani eneo la Obo, katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Anasema hofu ya LRA ni halisi kwa watu wa Afrika ya Kati hasa katika maeneo ya vijijini ambako kuna msitu mkubwa na hakuna mpaka unaofahamika kati ya Uganda ya Afrika ya Kati,Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, na pia Sudan Kusini.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.