Chen Hakulazimishwa kuondoka-Locke

Chen Guangcheng Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Chen Guangcheng akiwa hospitalini

Balozi wa Marekani mjini Beijing, amesema kuwa mwanaharakati wa kijamii kutoka China, Chen Guangcheng, hakushurutishwa kuondoka kutoka ubalozi wake.

Amesema mwanaharakati huyo alitaka kuondoka kutoka majengo ya ubalozi huo, kwa hofu ya usalama wake na familia yake.

Chen, amesema aliondoka kutoka hifadhi yake katika ubalozi wa Marekani, baada ya maafisa wa China kutishia usalama wa familia yake.

Lakini balozi wa Marekani, Gary Locke amesema Bwana Chen, alionekana kuwa na hamu ya kuondoka kutoka ubalozi huo.

Suala hilo lingali linaangaziwa pakubwa na vyombo vya habari kuliko mazungumzo kati ya maafisa wakuu wa serikali ya Marekani na China yanayoendelea mjini Beijing ambayo yalihudhuriwa na waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bi Hillary Clinton.

Chen ataka Obama kumsaidia

Katika mahojiano na shirika la habari la CNN, Bwana Chen, ametoa wito kwa rais wa Marekani, Barrack Obama kumsaidia.

''ningependa kumueleza rais Obama, tafadhali fanya kila juhudi ili kusaidi familia yangu kuondoka nchini China'' alisema bwana Chen.

Siku ya Jumatano, ilionekana kuwa Marekani iliafikiana mkataba ambao ungemaliza mzozo wa kidiplomasia kati yake na China.

Awali Bwana Chen alikariri kuwa hakuwa na nia ya kuondoka nchini humo.

Lakini akiwa katika hospitali moja mjini Beijing, mwanaharakati huyo ameonekana kubadili msimamo wake.

Kwa mujibu wa ripoti, Chen alichukuwa uamuzi huo baada ya kuelezwa na mkewe kuwa alidhulumiwa na maafisa wa polisi wa China wakati alipokuwa mafichoni katika ubalozi wa Marekani.

Lakini sasa Serikali ya Marekani, imejipata kati hali ya njia panda.

Maafisa waandamizi wa Marekani wanasema, watajadiliana zaidi kuhusu suala hilo na Bwana Chen, ili kutambua kile anachotaka.

Maafisa hao wanafahamu wazi kuwa ni sharti walishughulikie suala hilo kwa umakini, ili wasihujumu zaidi uhusiano wao na utawala wa Beijing.