Mke aliyesalitiwa ararua mavazi yake

John Edwards Haki miliki ya picha AP
Image caption John Edwards akitoka mahakamani

Mahakama moja Nchini Marekani, imefahamishwa kuwa mkewe aliyekuwa mgombea wa kiti cha urais, John Edwards, Elizabeth Edwards alirarua mavazi yake baada ya kugombana na mumewe kuhusu madai kuwa alikuwa akishiriki mapenzi nje ya ndoa.

Shahidi mmoja aliambia mahakama hiyo kuwa Bi Elizabeth, ambaye anaugua saratani ya matiti, alizirai wakati wawili hao walipogombana katika eneo la kuegeshea magari katika uwanja wa ndege.

Mwanawe wa kike mwenye umri wa miaka 30, ambaye ni wakili aliondoka mahakamani akilia wakati shahidi wa mwisho alipokuwa akitoa ushahidi wake, kuhusu kesi inayomkabili bwana Edwards ya kutumia fedha za kampeini kinyume cha sheria.

Edwards asema hana hatia

Bwana Edwards amekanusha madai ya kutumia fedha za kampeini kumficha mpenzi wake ambaye alikuwa mja mzito.

Ikiwa atapatikana na hatia, Edwards huenda akahukumiwa kifungo cha hadi miaka 30 gerezani.

Edward vile huenda akapigwa faini ya $1.5m.

Hata hivyo Edwards amekanusha mashtaka sita yanayomkabili kuhusu utumizi mbaya wa fedha za kampeini.

Mshauri wa zamani wa mawasiliano wa Bwana Edwards, Christina Reynolds ambaye ni pia mshirika wa karibu wa mkewe Edwards, alifahamisha mahakama hiyo jinsi wawili hao walipogombana nje ya duka moja la jumla, baada ya jarida moja kuchapisha habari kuwa bwana Edwards alikuwa akishiriki mapenzi nje ya ndoa.

Jarida hilo la National Inquirer, lilichapisha habari kuhusu uhusiano wa kimapenzi kati ya Bwana Edwards na Rille Hunter ambaye hatimaye alikuwa mja mzito.

Bi Reynolds, mwenye umri wa miaka 37, alisema wawili hao walizomeana katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Raleigh-Durham katika jimbo la North Carolina mwaka wa 2007.