Japan yazima vinu vya nuklia

Japani inafunga kinu chake cha mwisho cha nuklia kilichokuwa bado kinafanya kazi, na hivo nchi kuwa haitumii nishati inayotokana na nuklia kwa mara ya kwanza kwa miongo mine.

Kinu hicho - kwenye mtambo wa Tomari, kaskazini mwa Japani - ndio cha mwisho kati ya vinu zaidi ya 50 ambavyo vimezimwa ili kufanyiwa ukarabati, tangu tetemeko la ardhi na tsunami ya mwaka jana, ambayo ilipelekea kinu cha Fukushima kuripuka.

Serikali ya Japani itapenda kuendelea kutumia nishati ya nuklia, lakini serikali za mitaa nchini zimekataa vinu hivo kuanza tena kutumika.

Japani imekuwa ikinunua gesi nyingi kutoka nchi za nje ili kukidhi mahitaji yake ya umeme, lakini kuna wasiwasi umeme ukiwa haba na ghali utaathiri vibaya uzalishaji wa bidhaa viwandani.