Amri ya kutotembea ovyo yamewekwa-Misri

Wanajeshi wa Misri wakilinda makao makuu ya wizara ya ulinzi Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wanajeshi wa Misri wakilinda makao makuu ya wizara ya ulinzi

Amri ya kutotembea ovyo usiku tayari imeanza kutumika nchini Misri, katika eneo linalozunguka wizara ya ulinzi mjini Cairo kufuatia mapigano yaliyozuka kati ya waandamanaji na vikosi vya usalama hapo jana.

Ghasia hizo zilizuka baada ya waandamanaji kupuuza onyo la jeshi la kutokaribia eneo la wizara hiyo ya ulinzi na kuanza kulishambulia jengo la wizara hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa ya serikali, mwanajeshi mmoja ameaga dunia kutokana na majeraha huku mamia ya watu wakiwa wamejeruhiwa.

Waandamanaji kadha wamekamatwa na maafisa wa ulinzi na kwa sasa wanazuiliwa katika vituo mbali mbali vya kijeshi.

Waandamanaji wamelilaumu Baraza Tawala la Kijeshi la Misri, kwa kuchochea shambulio dhidi ya waandamanaji, Jumatano wiki hii ambapo watu wapatao 20 waliuawa na watu waliokuwa wamejihami kwa silaha.

Ghasia hizo zinatokea ikiwa ni wiki tatu tu zimebakia kabla ya kufanyika uchaguzi wa kwanza wa rais tangu Hosni Mubarak ang'olewe madarakani, ambapo Baraza la Kijeshi limetangaza kuwa litamkabithi madaraka atakayeshinda uchuguzi huo wa urais.