Ufaransa na Ugiriki zachagua viongozi

Upigaji kura unaendelea leo katika nchi kadha za Ulaya, ukigubikwa na matatizo ya Umoja wa Ulaya.

Haki miliki ya picha AFP

Wananchi wa Ufaransa wanachagua rais.

Lakini uchaguzi wa wabunge wa Ugiriki ndio unaweza kuwa na athari kubwa katika msususko wa kiuchumi wa Ulaya.

Serikali za nchi za Ulaya zinapambana na matatizo ya kiuchumi kwa namna mbali-mbali; pamoja na kupunguza kasoro kubwa kwenye bajeti zao, na kuzuwia makosa hayo yasirudiwe tena.

Uchaguzi wa juma hili unaweza kuathiri yote mawili.

Msukosuko ulianza Ugiriki.

Na hatua ya mwanzo iliyochukuliwa ni kubana matumizi ili serikali iweze kupunguza deni lake.

Iwapo uchaguzi utaleta serikali isiyotaka kuendelea kukaza mkaja, basi wafadhili wa Ugiriki, yaani mataifa mengine ya Ulaya pamoja na IMF, hawatakubali kuendelea kuiokoa Ugiriki.

Na katika uchaguzi wa Ufaransa, mgombea wa mrengo wa kushoto, Francois Hollande, anataka nchi iache kubana matumizi na badala yake ichukue hatua za kukuza uchumi.

Masoko ya fedha yanaona Bwana Hollande hatofanya mabadiliko ya kimsingi.

Ilivoelekea uchaguzi wa Ugiriki ndio unaweza kuwa changa moto kubwa katika hali ya uchumi ya sasa bara la Ulaya.