Marekani yatibua njama ya kulipua bomu

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Waziri wa ulinzi Marekani, Leo Panetta

Marekani imetibua njama ya kundi la kigaidi la al-Qaeda katika ufuo wa Arabia ya kulipua bomu sawa na alililokuwa nalo mtu aliyejaribu kulipua ndege ya shirika moja la Marekani iliyokuwa ikitoka Yemen kuelekea Marekani mwaka 2009.

Hata hivyo majasusi wanasema bomu lililopatikana lilikuwa la hali ya juu kuliko lile la mwaka 2009.

Maafisa wanasema jaribio hilo lilikuwa limepangwa na kundi moja lenye uhusiano na kundi la al-Qaeda nchini Yemen, na lilipangwa kutekelezwa wakati wakiadhimisha mwaka mmoja tangu kuuawa kwa Osama Bin Laden.

Bomu hilo lilinaswa nchini Yemen wakati wa operesheni ya majasusi wa CIA na FBI na linafanyiwa uchunguzi zaidi nchini Marekani.

Kufuatia ushirikiano na washirika wao wa usalama kwingineko, taarifa ya FBI, ilisema kuwa majasusi wamefanikiwa kutibua njama ya shambulizi la kigaidi.

Duru zinaarifu kuwa hakuna eneo lolote mahsusi lilikuwa limelengwa na kwamba hakuna tikiti za ndege zilikuwa zimenunuliwa wakati bomu lilinaswa wakati njama ilipotibuliwa.

Maafisa wanasema kuwa hapakuwa na tisho lolote kwa umma. Hata hivyo haijulikani hatua zilizochukuliwa dhidi ya mshukiwa wa njama hiyo.

Bomu hilo ni sawa na lile lilikuwa limeshonewa ndani ya suruali ya mshambuliaji wa kujitoa mhanga raia wa Nigeria amabye alijaribu kulilipua mjini Detroit siku ya Krismasi mwaka 2009 lakini akashindwa.

Inaarifiwa kuwa bomu hilo lilinaswa siku kumi zilizopita. Waziri wa ulinzi Leo Ppanetta, alisema kuwa nchi hiyo inastahili kuwa chonjo dhidi ya walio na nia ya kushambulia Marekani na kwamba maafisa wa usalama watafanya kila wawezalo kuilinda nchi hiyo.