Maofisa waliangusha soko la hisa

Mashua ya anasa Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mashua ya anasa

Mratibu wa masuala aya fedha nchini Nigeria amedhihirisha kua maofisa wa ngazi ya juu wa soko la hisa walitumia dola milioni moja kwa kununulia saa 165 aina ya Rollex pamoja na mashua ya anasa(Yatch).

Katika taarifa iliyowasilishwa mbele ya kikao maalum cha bunge, mkuu wa tume ya hati za mikopo ya serikali, Aruma Oteh, alisema kua matumizi ya fedha kiholela yalisababisha soko la hisa kuathirika vibaya mno mnamo mwaka 2008 na bado lhaliaminiki na waekezaji.

Image caption Soko la Hisa Nigeria

Bw.Arunma Oteh anasema kua biashara ya ndani, ubadhirifu katika kupanga bei za hisa na matumizi mabovu ya fedha ya wakuu wa soko la hisa la Nigeria kulisababisha kuanguka kwa soko hilo.

Arunma Oteh alikifahamisha kikao cha bunge kua, pamoja na ubadhirifu huo, maofisa hao walitumia sehemu ya pesa hizo kununulia saa 165 aina ya Rollex kama zawadi kwa wenzao waliokua wanaondoka.

Kiongozi huyo aliongezea kusema kua pamoja na mashua ya anasa iliyonunuliwa na nusu ya idadi ya saa hizo haijulikani zilipo.

Aliyekua mkuu wa soko hilo la hisa, Ndi Okereke-Onyiuke, amekanusha madai hayo na kusema kua soko hilo liliklua kampuni baki isiyo ya serikali, yenye uwezo wa kutumia fedha zake inavyotaka.

Bibi huyo ametetea kipindi alipokua kiongozi wa soko la hisa akisema kua soko hilo la hisa lilikua imara bila tatizo lolote.

Bi.Okereke-Onyiuke alifutwa kazi mnamo mwaka 2010 kufuatia mageuzi ya sekta ya fedha.

Arunma Oteh amefanya juhudi kali za kusafisha masoko ya Nigeria. Lakini wakosoaji wanamlaumu kwa mratibu huyo kwa kuwakaripia wasiohusika.

Ni Majuma machache tu yamepita ilipotokea sarakasi ndani ya bunge wakati wa kikao ambapo Bi.Oteh na mkuu wa kamati ya bunge walirushiana matusi na madai ya rushwa huku Televisheni ikirusha matangazo ya moja kwa moja.

Arunma Oteh aliteuliwa kama mratibu wa fedha nchini Nigeria mwaka 2010 akiahidi kutaja wahusika waliosababisha kuanguka kwa soko la hisa.

Hata hivyo raia wengi wanahisi kutaja na kuaibisha wahusika haitoshi. Kufuatia mgogoro wa kiuchumi nchini humo, Benki kuu ililazimika kuzinusuru benki tisa, na licha ya kufilisika ni mkuu mmoja wa benki aliyekabwa na sheria na kupelekwa jela.

Kikao cha hivi sasa kuhusu kuanguka kwa soko la hisa,ikiwa ni sehemu tu ya upelelezi unaofanywa kwa juhudi za kusafisha mfumo wa fedha za umma kinafuatiliwa kwa karibu mno na raia wa Nigeria.

Kila kukicha, raia wanaotazama maendeleo hayo kupitia runinga wanaomba dua waone wakiishi katika nchi isiyokua na rushwa,ufisadi na iwe ya kuaminika.